Na Mwandishi wetu, TADB
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ( TADB) kwa kuleta mageuzi makubwa ya Kilimo nchini.
Amesema hayo leo tarehe 3 Agusti, 2025 mara baada ya kutembelea banda la Mdhamini Mkuu wa Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima maarufu kama Nanenane ambaye ni TADB.
"Ninawapongeza TADB kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuchagiza maendeleo ya Sekta ya Kilimo na Ufugaji kwani ndiyo uti wa mgongo wa taifa letu na imeajiri zaidi ya asilimia 65 ya wananchi," alisisitiza Mhe. Majaliwa
Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Taasisi Bwana Waziri Mkani amesema kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka kumi ya TADB tangu kuanzishwa kwake 2015, Benki hiyo imepata mafanikio mengi, ikiwa ni pamoja na ukuaji benki toka benki ndogo hadi kufikia benki kubwa katika utoaji wa huduma za kifedha nchini.
"Benki ilianza na mtaji wa bilioni 60, lakini hivi leo benki imetoa mikopo yenye thamani ya tirilioni 1.129 ambayo ni mafanikio makubwa yanayotokana na utashi wa Serikali wa Awamu ya Sita iliyowekeza kwenye Sekta ya Kilimo na Mifugo kwa ajili ya kuwakomboa wakulima ambao walikuwa hawapati fursa ya mikopo yenye riba ndogo awali" amesema Mkani.
Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yanaenda sambamba na kaulimbiu inayosema " Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025.