
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa rai kwa wadau wa mazingira katika ngazi zote na wananchi kwa ujumla kuungana na Serikali kwa hali na mali katika mapambano dhidi ya kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
Pia, amewaomba wananchi kuendelea kupanda miti na kuitunza ili kukabiliana na athari za ukame ambao unaathiri sekta mbalimbali ikiwemo maji, mifugo na kilimo ambazo zina umuhimu mkubwa kwa binadamu.
Ametoa wito huo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani yaliyofanyika kitaifa leo tarehe 17 Juni, 2025 katika Manispaa ya Shinyanga.

Alisema Tanzania ni moja ya waathirika wa hali ya ukame hivyo Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha inakabiliana na tatizo hilo kwa ufanisi mkubwa kwa kushirikisha wizara za kisekta, taasisi za umma, washiriki wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi na taasisi za kidini.




