Breaking

Tuesday, 15 March 2022

MCHUNGAJI ANAYEDAI KUFUFUA WATU AKAMATWA NA POLISI




Na Mwandishi Wetu - Shinyanga

JESHI la Polisi Mkoani Shinyanga linamshikilia Mchungaji wa Kanisa la CRTC, Yohana Nyasilu (34) kwa tuhuma za kudai anafufua watu waliokufa kwa lengo la kuvuta watu katika kanisa lake ili lipate waumini wengi.


Mbali ya mchungaji huyo pia Jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Yohana Komanya (21) ambaye hata hivyo makazi yake hayakufahamika mara moja kwa kujifanya Msukule aliyefufuliwa na Mchungaji huyo.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP George Kyando amesema kuwa mnamo Machi 13, 2022 Jeshi la polisi Mkoani humo lilipokea taarifa za kuwepo kwa Mchungaji anayedai kufufua watu kwenye kijiji na kata ya Puni wilayani Shinyanga.


Kamanda Kyando amesema baada ya kupata taarifa hizo Jeshi la Polisi lilienda katika kata hiyo ambako umati wa watu walikuwa wamekusanyika kushuhudia miujiza ya kufufua wafu iliyokuwa ikifanywa na mchungaji huyo.


“Ni kweli jamii ya watu wengi wa kijiji cha Puni walitaharuki, walijaa sana kushuhudia kile alichokuwa akikifanya na waliamini ni mtu mwenye uwezo wa kufufua wafu, hata hivyo mtu aliyedaiwa kufufuliwa baadaye alimgeuka mchungaji kwa kudai alimshawishi adai kwamba alikuwa amekufa na kufufuliwa na Mchungaji huyo wa Kanisa",amesema Kamanda Kyando.


“Lengo lake lilikuwa kuvuta watu wengi na kiini cha kupata watu wengi kanisani ni kupata sadaka nyingi, nia ni kipato, hivyo tunamshikilia mchungaji huyu na uchunguzi ukikamilika jalada litapelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali kuona wachungaji wa namna hii wanachukuliwa hatua gani,” ameongeza Kamanda Kyando.


Kamanda Kyando ametoa wito kwa watu wa madhehebu yote ya dini kujihadhari na uongo na udanganyifu unaoweza kuwaletea taharuki kwenye jamii na kwamba tayari jamii ya watu wa Puni ilishataharuki na kuamini kweli mchungaji huyo alikuwa na uwezo wa kufufua wafu.


“Jeshi la Polisi kwa upande wetu hatutaacha kuwashughulikia watu wa dini wa aina hii maana yake kuleta taharuki kwenye jamii yetu ni kitu ambacho hakiruhusiwi kwenye jamii yetu, na kwa taarifa nilizonazo tukio hili si la mara ya kwanza kwa mchungaji huyu,” ameeleza Kamanda Kyando.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages