Breaking

Tuesday, 15 March 2022

TARURA YATAKIWA KUTUMIA FEDHA ZA MIRADI KWA USAHIHI ILI KUPATA BARABARA ZENYE UBORA




Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) imetakiwa kuhakikisha miradi inayotumia fedha za Serikali na wafadhili ilenge maeneo husika ili kupata barabara zenye viwango na ubora unaotakiwa.


Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Abdalah Chaurembo leo tarehe 15 Machi, 2022 wakati wa ziara ya Kamati hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rugwe, kuangalia miradi inayotekelezwa na Serikali hasa katika sekta ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika halmashauri hiyo.


Chaurembo amesema ili barabara ziweze kukidhi mahitaji kwa wananchi na kudumu kwa muda mrefu zinatakiwa kuwa na viwango vya ubora vinavyotakiwa.


Aidha amewataka Mameneja TARURA katika wilaya zote kutoa ushirikiano kwa Wabunge na ushauri wa kitaalam kabla ya kutekeleza miradi katika maeneo yao ili miundombinu hiyo iweze kuendana na uhitaji wa maeneo huska.


Pia ameipongeza Serikali TARURA Mkoa wa Mbeya kwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa Barabara ya Masebe – Bugoba- Lutete yenye urefu wa kilometa 7.2 na barabara ya Masebe DSP-Mpuguso TTC –Bukoba yenye urefu wa kilometa 5.0 zilizojengwa kwa kiwango cha lami katika Halmashauri ya Wilaya ya Rugwe Mkoani humo.



Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa ameendelea kuwasisitiza TARURA wanapoandaa BoQ wazingatie mpango wa kuweka taa za barabarani kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa kwa TARURA nchi nzima.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages