Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mojawapo ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ambazo zinashiriki katika Mkutano wa Tisa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika unaojulikana kama TICAD 9.
Mkutano wa TICAD 9 Summit, umefunguliwa leo tarehe 20 Agosti 2025 kwa pamoja na Mheshimiwa Shigeru Ishiba, Waziri Mkuu wa Japan; Mheshimiwa João Lourenço, Rais wa Jamhuri ya Angola na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU); Mheshimiwa António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN); Mheshimiwa Mahmoud Ali Youssouf, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC); Bw. Haoliang Xu, Acting Administrator and UNDP Associate Administrator; na Bw. Makhtar Diop, Mkurugenzi Mtendaji wa International Finance Corporation (IFC) kwa niaba ya Rais wa Benki ya Dunia.
Katika hotuba ya ufunguzi ya Waziri Mkuu wa Japan, Japan imeahidi kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na Nchi za Afrika katika maeneo makuu matatu ya: Uchumi, Jamii, Ulinzi na Usalama.
Mahususi kabisa Japan imeahidi kushirikiana na Afrika katika kutatua changamoto za madeni yasiyohimilika; kuimarisha mtangamano wa Afrika; ushirikiano wa kikanda kupitia utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA); kukuza sekta binafsi ya Afrika kwa kuwezesha ushirikiano na sekta binafsi ya Japan; kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu hususan katika kuwezesha vijana na wanawake kupitia program za mafunzo, startups, na kuunga mkono juhudi za Afrika za Huduma Bora ya Afya kwa watu wote.


