
Serikali imesema wiki ijayo itatangaza nafasi za ajira 32,000 katika sekta ambazo zina upungufu mkubwa wa watumishi.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Aprili 6, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Jenista Mhagama Bungeni Jijini Dodoma.
Hayo yamekuja baada wabunge kuuliza maswali mengi ya nyongeza yaliyoulizwa katika Wizara ya Tamisemi wakitaka kujua namna ambavyo Serikali itapeleka watumishi kuziba nafasi katika vituo vingi vya sekta ya afya na elimu vilivyojengwa nchini.
Akijibu Maswali hayo Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, David Silinde amesema wizara hiyo ingetoa tangazo la ajira na mgawanyiko wake na kuomba wabunge kuwa watulivu.
Kwa upande wake Waziri Mhagama akitoa amesema Rais ameridhia na kutoa kibali cha kuajiri watumishi elfu 32,000 na wiki ijayo atazitangaza.
“ Serikali ilipanga kuajiri watumishi 44,000 kwa mwaka huu wa fedha, na tayari tumeshaajiri watumishi 12,000 na sasa nitangaze kuwa wiki ijayo nitatangaza ajira 32,000,” amesema Mhagama.