.jpeg)
Na Samir Salum - Lango la habari
Serikali imewaelekeza wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa muhimu kushusha mara moja bei za bidhaa walizopandisha pasipo kuendana na uhalisia wa soko ikiwa ni pamoja na kutotumia kipindi hiki cha Ramadhani na Kwaresma kupandisha bei.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano April 06, 2022 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2022/2023 Bungeni Dodoma.
Waziri Mkuu amesema hivi karibuni kumekuwepo na taarifa za uhaba na upandaji wa bei usioendana na uhalisia wa soko kwenye bidhaa za ujenzi, vyakula, nishati na pembejeo za kilimo ambapo aliielekeza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuunda jopo la Wataalamu ili kufuatilia taarifa hizo.
Amesema kuwa Wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Tume ya Ushindani ilifanya ufuatiliaji na tathmini ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu zinazozalishwa nchini na zile zinazotumia malighafi kutoka nje ya nchi.
Amesema Kutokana na ufatiliaji huo Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na upandaji huo wa bidhaa muhimu ikiwa ni pamoja na usimamiaji wa Sheria ya Ushindani Na. 8 ya Mwaka 2003 ambayo inazuia kupanga bei.
Ameongeza kuwa Serikali imechukua hatua kutafuta vyanzo mbadala vya upatikanaji wa bidhaa na kuweka mifumo ya kusimamia masoko ya awali na minada.
"Serikali inawaelekeza wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa muhimu kushusha mara moja bei za bidhaa walizopandisha pasipo kuendana na uhalisia wa soko ikiwa ni pamoja na kutotumia kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresma kupandisha bei" Amesisitiza Waziri Mkuu
Aidha amewasihi wazalishaji na wafanyabiashara wa bidhaa muhimu kuuza bidhaa husika kwa kuzingatia gharama halisi za uingizaji, uzalishaji na usambazaji.
"watakaobainika kupandisha bei bidhaa muhimu bila utaratibu hatua kali zitachukuliwa dhidi yao" Ameonya Waziri Mkuu