Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Timothy Ndaya amewataka wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu na ujenzi katika wilaya hiyo kufuata sheria za madini pamoja na kanuni mbalimbali zilizowekwa na Serikali ili uchimbaji wao uinue uchumi wa nchi bila kuleta athari zozote.
Ndaya ameyasema hayo leo Ijumaa Machi 11, 2022 Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama wakati akifungua mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini na viongozi wanaosimamia maeneo ya uchimbaji wa madini kuhusu usimamizi wa usalama, afya na mazingira kwenye migodi yaliyoendeshwa na Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira iliyopo chini ya Tume ya Madini yaliyofanyika Kahama mkoani Shinyanga.
Amesema kuwa migogoro mingi imekuwa ikitokea katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini kutokana na wananchi wengi kutokuwa na uelewa kuhusu sheria ya madini na kanuni zake hasa kanuni ya usalama, afya na usimamizi wa mazingira.
Ameongeza kuwa kutokana na changamoto ya uharibifu wa mazingira na uelewa mdogo wa sheria ya madini kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, Serikali kupitia Tume ya Madini imeanza kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini ili kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa kufuata sheria na kanuni za madini na kuepuka migogoro na ajali zinazotokea migodini.
"Ni vyema mkahakikisha mnafuata sheria na kanuni za madini, miongozo mnayopewa na Serikali na mafunzo yanayotolewa ili uchimbaji wenu ulete manufaa kwenu binafsi bila kusababisha ajali na kuleta athari kwenye mazingira," amesema Ndaya.
Aidha ameshauri ujenzi wa mitambo ya kuchenjua madini katika eneo moja ili kurahisisha usimamizi wake na kupunguza athari za mazingira.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Henry Mditi amesema kuwa, maeneo yanayoangaziwa katika mafunzo hayo ni pamoja na usalama migodini, utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya madini usimamizi wa baruti, usimamizi wa mitambo ya uchenjuaji wa madini pamoja na sheria ya madini na kanuni zake.
Ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni pamoja na kuongeza uelewa mpana wa shughuli za migodi, sheria ya madini hivyo kupunguza matukio ya ajali kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.
"Kumekuwepo na changamoto ya uharibifu wa mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na ajali ndio maana tumekuwa tukiendesha mafunzo kama haya sehemu mbalimbali nchini," amesisitiza Mhandisi Mditi.
Amesisitiza kuwa mafunzo yameshatolewa katika mikoa ya kimadini ya Mirerani, Chunya, Simiyu, Singida, Dodoma na yatakuwa endelevu ambapo yataendelea kutolewa katika mikoa mingine ya kimadini iliyobaki.
Mafunzo hayo yametolewa na wataalam ambao ni viongozi waandamizi wa Tume ya Madini wakiwa ni pamoja na Meneja wa Ukaguzi wa Migodi, Winfrida Mrema, Meneja wa Usimamizi wa Baruti, Mhandisi Aziza Swedi, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Dkt. Anorld Gesase na Afisa Mazingira Mwandamizi, Abel Malulu.