Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, ameutaka uongozi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mzenga, kilichopo Kata ya Mzenga, Wilaya ya Kisarawe, kuhakikisha kinatoa mafunzo katika fani zinazoendana na shughuli za kiuchumi za eneo hilo.
Mhe. Wanu ametoa agizo hilo Machi 03, 2026, wilayani Kisarawe wakati wa ziara ya ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na Wizara katika wilaya hiyo.
Amewataka viongozi wa wilaya na wananchi wa eneo hilo kuona umuhimu wa mafunzo ya ujuzi na hivyo kuhamasisha vijana kujiunga na chuo hicho ili kupata ujuzi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Amesema chuo hicho, pamoja na vyuo vingine vya maendeleo ya wananchi, vinapaswa kuzingatia mahitaji halisi ya kiujuzi ili vijana waweze kujiunga kwa wingi.
“Mmesema hapa mnazalisha zao la korosho, ufuta na mihogo; kwa nini sasa msianzishe kozi ya kusindika mazao hayo? Hii itawamasisha vijana kujiunga na chuo kwa kuwa wanasoma kile wanachofanyia kazi,” amesema Mhe. Wanu.
Aidha, ameutaka uongozi wa chuo hicho kusimamia ipasavyo mifumo ya usimamizi wa watumishi ili kuimarisha uwajibikaji.
Akiwa wilayani humo, Mhe. Wanu pia amekagua ujenzi wa VETA Kisarawe na kusema kuwa Serikali inaendelea kujipanga kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa chuo hicho ili malengo ya kutoa ujuzi kwa wananchi yafikiwe.









