Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Kifaransa Tanzania (TAFT), Constantin Njalambaya, akizungumza na walimu wa somo la Kifaransa Siku ya Walimu wa Kifaransa Duniani (International French Teachers’ Day – IFTD) yaliyofanyika novemba 22, 2025 Ngara Kagera.Na Neema Nkumbi, Ngara Kagera
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Kifaransa Tanzania (TAFT), Constantin Njalambaya, ameongoza maadhimisho ya Siku ya Walimu wa Kifaransa Duniani (IFTD) 22 Novemba 2025 wilayani Ngara, katika hafla iliyobeba kaulimbiu “Kuimba, Kucheza, Kufundisha: Lugha ya Kifaransa katika Muziki.”
Katika hotuba yake, Njalambaya ametambua mchango mkubwa wa walimu wa Kifaransa nchini, akiwapongeza kwa kujitolea kuendeleza lugha hiyo licha ya changamoto za rasilimali, mazingira magumu ya kazi na umbali wa shule, amesema walimu hao ni mabalozi wa lugha, utamaduni na mshikamano, na wanastahili kupewa msaada zaidi.
Ngara imechaguliwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya mwaka 2025 kutokana na mchango wake mkubwa katika ufundishaji wa Kifaransa, ikiwa ndiyo Wilaya yenye idadi kubwa zaidi ya shule zinazofundisha somo hilo, pamoja na historia ya walimu kujitoa kwa kiwango cha juu katika mazingira yenye changamoto.
Kaulimbiu ya mwaka huu imeangazia nafasi ya muziki katika ufundishaji wa lugha, kufuatana na mwongozo wa Shirikisho la Kimataifa la Walimu wa Kifaransa (FIPF), Njalambaya amesema muziki ni nyenzo muhimu inayowezesha ubunifu, ushirikishwaji na kujenga mawasiliano ya kina katika ujifunzaji wa lugha.
Aidha, Njalambaya ametoa shukrani kwa Ubalozi wa Ufaransa kwa msaada wa kifedha uliowezesha kufanyika kwa maadhimisho hayo, akibainisha kuwa msaada huo unaimarisha dhamira ya kukuza na kuendeleza ufundishaji wa Kifaransa nchini.
Wito kwa Walimu na Wawezeshi wa Lugha
Walimu mstaafu wa Kifaransa, Andrea Isaya, amewahimiza walimu wanaofundisha lugha hiyo kuendelea na juhudi zao, na kuwataka wawezeshi wa lugha kuhakikisha walimu wanapata semina, vitabu na vifaa vya kujifunzia.
Viongozi wa dini, akiwemo Sheikh Ramadhani Hussein wa Ngara Mjini, wamesisitiza kuwa walimu wanasimama imara katika ufundishaji ili watoto waweze kuwasiliana kikamilifu kibiashara na kitaaluma wanapokua.
Padri Denis ameongeza kuwa kumpa mtu elimu ya lugha ni sawa na kumpa ufunguo wa maisha.
Katibu wa Chama cha Walimu Wilaya ya Ngara, Amani Zephania, amesema chama hicho kitaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha walimu wanapata mafunzo endelevu, vifaa vya kufundishia na mazingira bora ya kazi, huku akiwataka wadau na serikali kuongeza uwekezaji katika ufundishaji wa lugha za kigeni, ikiwemo Kifaransa, kwa manufaa ya kizazi kijacho.
Katibu Mkuu wa TAFT, Ally Saleh, ameeleza kuwa ubalozi unatoa vitabu vya Kifaransa na amewahimiza walimu kujiunga na chama cha walimu wa Kifaransa ili kupata semina na mafunzo zaidi.
Maadhimisho hayo yamehitimishwa kwa wito wa kuimarisha umoja, ubunifu na mshikamano miongoni mwa walimu wa Kifaransa nchini, huku Ngara ikitajwa kubaki katika kumbukumbu kama mahali palipojenga ari mpya ya kuikuza lugha ya Kifaransa Tanzania.
















