Naibu Katibu Mkuu TUGHE Taifa, Ndg. Amani Msuya ameeleza kuvutiwa na kiwango cha utendaji kazi wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa mwaka 2024/25 kufuatia Mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake kwa zaidi ya asilimia 94.
Msuya ameeleza hayo Oktoba 27, 2025 Mkoani Morogoro wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi PURA kilichofanyika kwa lengo la kujadili, pamoja na mambo mengine, taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25.
“Nimevutiwa sana kusikia kuwa, kwa mujibu wa mrejesho wa tathmini ya utekekelezaji wa mjukumu iliyofanywa kupitia Mfumo wa Tathmini ya Utendaji kazi (PEPMIS), PURA ilitekeleza majukumu yake kwa asilimia 94.46 kwa mwaka wa fedha 2024/25”
“Kwa kiwango hiki cha utendaji kazi, ni dhahiri kuwa PURA inatekeleza majukumu yake ipasavyo na kwa hakika ni jambo linalostahili pongezi” alisema Msuya.
Msuya pia alitumia fursa hiyo kuwaasa watumishi wa PURA kutobweteka na kiwango cha tathmini cha mwaka wa fedha uliopita na badala yake waendelee kufanya kazi kwa juhudi zaidi ili kuongeza kiwango kwa mwaka 2025/26.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Charles Sangweni alisema kuwa PURA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa juhudi zaidi, weledi na ubunifu kwa kuzingatia mipango ya Taasisi.
Sangweni pia alitoa rai kwa watumishi wa PURA kuendelea kuzingatia ujazaji wa taarifa za utendaji kazi katika PEPMIS kwa kuwa taarifa hizo ni moja ya nyenzo muhimu zinazotumika katika masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwemo kupandishwa vyeo.



Naibu Katibu Mkuu TUGHE Taifa, Ndg. Amani Msuya akichangia jambo wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi PURA kilichofanyika Oktoba 27, 2025 Mkoani Morogoro.







