Breaking

Thursday, 12 February 2026

MWENYEKITI WA BODI YA NEMC AZINDUA MWALO WA MFANO KWA WACHIMBAJI WADOGO WA DHAHABU – GEITA

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mhandisi Mwanasha Tumbo, amezindua mwalo wa mfano wa uchenjuaji wa dhahabu kwa wachimbaji wadogo wa Mgusu mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya uchimbaji na uchakataji madini pamoja na kudhibiti matumizi ya kemikali ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu.

Uzinduzi huo umefanyika wakati wa ziara ya kikazi ya Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Baraza mkoani Geita, kujiridhisha na masuala ya Mazingira kwa elimu ya matumizi ya teknolojia salama na rafiki kwa mazingira katika shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Mhandisi Mwanasha Tumbo alisisitiza umuhimu wa wachimbaji kuzingatia mbinu bora na salama katika shughuli zao ili kulinda afya zao, jamii inayowazunguka pamoja na mazingira kwa ujumla. Alieleza kuwa mwalo huo wa mfano utakuwa chachu ya mabadiliko kwa wachenjuaji na wachimbaji wengine kuiga mifumo bora ya uchakataji madini.

Katika ziara hiyo, Bodi pia ilitembelea eneo linalojengwa jengo la ofisi litakalotumika kama Kituo cha Uhamasishaji (

Awareness Centre) chini ya Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa Dhahabu (EHPMP). Kituo hicho kinatarajiwa kutoa elimu kwa wachimbaji na jamii kuhusu athari za zebaki na umuhimu wa kutumia teknolojia mbadala zisizo na madhara kwa afya na mazingira.

Aidha, wajumbe wa Bodi walipata fursa ya kuonana na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Reuben Shigella, ambaye alieleza kufurahishwa na ujio huo na kupongeza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Baraza na uongozi wa mkoa. Alisisitiza kuendelezwa kwa mahusiano hayo kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu na kulinda rasilimali za Taifa.

Kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za uhifadhi wa mazingira, Bodi ya NEMC, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita na Menejimenti walishiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la jengo la kituo hicho, wakionesha dhamira ya dhati ya kuimarisha utunzaji wa mazingira.

Ziara hiyo pia ilihusisha kutembelea mgodi wa Geita Gold Mining (GGM), ambapo wajumbe walijionea hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kulinda mazingira na kuendesha shughuli za uchimbaji kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

Kwa ujumla, ziara hiyo imeimarisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi, kuimarisha ushirikiano na wadau pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia salama katika sekta ya uchimbaji mdogo wa dhahabu.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages