
Maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wamejitokeza kwa wingi kumsikiliza Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika leo Jumatano Septemba 3, 2025, Jimbo la Shinyanga Mjini.
Katika mkutano huo uliofurika umati wa wananchi, Dkt. Nchimbi amewanadi wagombea wa ubunge wa mkoa huo akiwemo Mhe. Patrobas Katambi (Shinyanga Mjini), Mhe. Lucy Mayenga (Kishapu), Mhe. Ahmed Salum (Solwa), na Mhe. Azza Hillal Hamad (Itwangi), pamoja na wagombea udiwani.
Dkt. Nchimbi amewaomba wananchi kumpigia kura za kishindo mgombea Urais wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Wabunge na Madiwani wa chama hicho, akisisitiza kuwa kuchagua viongozi wote wa CCM kutaunda mnyonyoro thabiti wa uongozi utakaoharakisha maendeleo ya wananchi.
Akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2025–2030), Dkt. Nchimbi amesema imelenga kuboresha maisha ya wananchi katika sekta zote muhimu.
Ametaja miradi mipya itakayotekelezwa Jimbo la Shinyanga Mjini ikiwemo ujenzi wa Zahanati mpya 10, Vituo vya Afya 7 na Wodi 10 za wazazi. Sekta ya elimu itanufaika na shule mpya za msingi 7, madarasa 200, shule mpya za sekondari 6 na madarasa 288.
Katika sekta ya maji, ameahidi kuendelezwa kwa miradi ya maji kutoka Ziwa Victoria na ujenzi wa visima virefu, huku sekta ya viwanda ikipewa kipaumbele kwa kujengwa viwanda vya ngozi na kuchenjua madini ili kuinua uchumi wa wananchi wa Shinyanga.
Aidha, akizungumzia mpango wa siku 100 za kwanza baada ya ushindi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Nchimbi amesema serikali itaajiri walimu 7,000 wa Sayansi na Hisabati, watumishi wa afya 5,000 na kutoa mikopo ya shilingi bilioni 200 kwa wananchi.
Akirejea utekelezaji wa Ilani ya CCM (2020–2025), amebainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana yakiwemo ongezeko la bajeti ya Wizara ya Afya kutoka shilingi bilioni 900 hadi trilioni 1.6.
Katika Jimbo la Shinyanga Mjini pekee, ametaja mafanikio ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Ibadakuli kwa kilomita 2.2, ongezeko la vituo vya afya kutoka 5 hadi 6, zahanati kutoka 44 hadi 59, pamoja na kuimarishwa huduma za afya kupitia vifaa vipya vya CT-SCAN na X-Ray Digital.
Vilevile, shule za msingi zimeongezeka kutoka 77 hadi 92, sekondari kutoka 44 hadi 49, huku visima virefu vya maji vikiongezeka kutoka 2,618 hadi 3,456.
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Shinyanga Mjini, Mhe. Patrobas Katambi, ameeleza utekelezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo barabara, masoko, stendi mpya ya mabasi na upanuzi wa uwanja wa ndege.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amesema utekelezaji wa Ilani ya CCM umekuwa wa kiwango cha juu mkoani humo, na kusisitiza kuwa Shinyanga ni ngome ya CCM ambayo itashinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Elizabeth Maliganya alivyoamsha Shangwe Uzinduzi Kampeni za UCHAGUZI mkuu CCM Shinyanga
Saida Karoli akiamsha amsha Live uzinduzi wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025 CCM Shinyanga
Ng'wana Kang'wa akishambulia JUKWAA uzinduzi wa Kampeni za uchaguzi Mkuu 2025 CCM Shinyanga Mjini