Wakazi wa Sinza E, jijini Dar es Salaam, wamelalamikia kusitishwa kwa huduma za Serikali ya Mtaa wao, baada ya eneo lililokuwa makao ya ofisi hizo kuvamiwa na viongozi kuamriwa kuondoka bila kueleza ofisi mpya zitakazotumika.
Tangu Mei mwaka huu, eneo hilo limekosa huduma za serikali ya mtaa, hali inayowalazimisha wananchi kuishi bila huduma muhimu za kila siku zinazotolewa na serikali za mitaa.
Paul Luvinga, mkazi wa Sinza E, amesema wananchi hawakushirikishwa katika uamuzi huo, na barua ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo iliyoamuru kuondoka haikuonesha ofisi mpya zitakapohamia. “Huduma zimekatika. Hatuna pa kufuatilia masuala ya serikali ya mtaa, na hatujui barua hiyo inatufikisha wapi,” amesema.
Aidha, Luvinga amesema mkanganyiko umeongezwa na taarifa kwamba eneo hilo si mali ya Halmashauri, kinyume na hukumu ya Mahakama Kuu ya mwaka 2003 iliyoelekeza ofisi za serikali ya mtaa ziendelee kuwepo hapo.
Kwa upande wake, Robarth Ngoti, amesema hatua hiyo ni kudhalilisha wananchi: “Hata Rais Samia akisikia hili, lazima atasikitishwa. Serikali haiwezi kuhamishwa kiholela na huduma zikakatwa kana kwamba wananchi hawapo.”
Mwenyekiti wa Shina namba 8, Dorah Ndanshau, amesema: “Wananchi tupo gizani. Huduma zimesimama. Hata barua ya Mkurugenzi haioneshi ofisi zimehamia wapi. Hii ni sawa na kufukuza mpangaji bila kumpa sehemu ya kwenda.”
Michuzi Media ilipotaka kujua zaidi, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sinza E, Clement Kavishe, alikiri kuondolewa kwa ofisi hizo lakini hakuweka wazi zilipohamishiwa, huku Mtendaji wa mtaa huo, Amina Juma Mwinyimvua, akigoma kueleza na kukata simu.