Breaking

Friday, 1 August 2025

TADB YACHANGIZA MAGEUZI SEKTA YA KILIMO NCHINI

Na Mwandishi wetu, Dodoma

 Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa  kuleta mapinduzi ya kilimo kwa vitendo kupitia mikopo yenye riba nafuu na uwezeshaji wa wakulima wadogo na wa kati kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Hayo yamesemwa leo Agosti 1, 2025 katika viwanja vya NaneNane jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw.Frank Nyabundege wakati akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango alipotembelea banda la Benki hiyo kabla ya kufungua maonesho hayo Kitaifa.

"Zaidi ya wakulima milioni 1.95 wamefikia ndoto zao kupitia TADB, huku zaidi ya shilingi  trilioni 1.13 zikitolewa tangu 2015 kama mtaji wa mabadiliko kwa kilimo cha Tanzania", alisisitiza Nyabundege

Akifafanua Bw.Nyabundege amesema TADB si tu Benki ni nguzo ya matumaini, injini ya uzalishaji, na daraja la maendeleo kwa wakulima wa Tanzania.

Aidha, Benki hiyo ni mdhamini mkuu wa maonesho ya NaneNane Kitaifa yaliyofunguliwa leo Agosti 1, 2025 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Mpango.

Sambamba na Maonesho hayo, TADB inasherekea miaka 10 ya mafanikio tangu kuanzishwa kwake. Benki hiyo kwa sasa ni miongoni mwa benki kubwa nchini na imewezesha sekta ya kilimo kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages