
MENEJA wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kati Hawa Lweno,akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la EWURA katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika kiwanja cha Nzuguni jijini Dodoma.
Na Alex Sonna-DODOMA
MENEJA wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kati Hawa Lweno, amesema Mamlaka hiyo imeshirikiana kikamilifu na wadau mbalimbali katika maonesho ya Nanenane kwa lengo la kutoa elimu kuhusu huduma zinazodhibitiwa na EWURA.
Timu ya wataalamu kutoka sekta za umeme, petroli,gesi asilia, maji na usafi wa mazingira , gesi pamoja na huduma kwa wateja wapo katika banda la EWURA ikitoa elimu kuhusu kazi na huduma zinazofanywa na mamlaka hiyo, ikiwemo kutoa leseni, kudhibiti ubora wa huduma na kuhakikisha upatikanaji na matumizi sahihi na salama ya huduma za nishati na maji.
Lweno amesema wadau wengi wamefika kupata elimu na kutoa maoni yao, wakiwemo wakulima, wadau wa nishati na maji, wamiliki wa vituo vya mafuta na wananchi wanaopata huduma za umeme na gesi.
Ameeleza kuwa changamoto kubwa ni upatikanaji wa mafuta vijijini, ambapo EWURA imekuwa imeweka masharti nafuu na kuendelea kutoa elimu kwa wakulima na wadau kuhusu namna ya kusogeza huduma hizo maeneo ya pembezoni jambo ambalo ameeleza kuwa limepata mwitikio mkubwa.
“Kwa mjini kituo kinaweza kuwa na mauzo ya hadi milioni 100 kwa siku na pampu nyingi, wakati vijijini kinaweza kufikia milioni 20 pekee na pampu moja tu, hivyo nitoe wito kwa watanzania hususani wakulima kuiona fursa hii” amesema.
Aidha, amesema EWURA imeendelea kuelimisha wananchi kuhusu taratibu za kupata leseni za kutoa huduma za nishati na maji, jambo ambalo limeongeza uelewa na hamasa ya wananchi wengi kutaka kufahamu zaidi.
Lweno pia amebainisha kuwa masuala ya maji yamekuwa miongoni mwa hoja zinazojitokeza zaidi katika maonesho hayo, ambapo baadhi ya wateja wameonesha wasiwasi kuhusu ubora wa maji wanayoyapata na EWURA imewahakikishia kuwa ubora wa maji ni eneo ambalo imekuwa ikilifuatilia kwa umakini.
Aidha amesema EWURA, imekuwa ikiwapa wananchi elimu kuhusu vigezo vya ubora na usalama wa maji.
Ametumia nafasi hiyo kutaka wananchi wote wanaotembelea maonesho ya Nanenane kufika katika banda la EWURA ili kupata elimu zaidi ya masuala ya udhibiti wa huduma za nishati na maji.








