Breaking

Thursday, 31 July 2025

RAIS SAMIA AIPA NEEMA MIRADI YA KUZALISHA UMEME IRINGA

   

📌Atoa zaidi ya bilioni 15 mradi wa Mwenga Hydro Ltd

📌Mwenga Hydro Ltd yaunganisha wateja 8,000 huduma ya umeme

📍Mufindi - Iringa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan  ametoa kiasi cha shilingi bilioni 15 kwenye mradi wa kuzalisha umeme wa Mwenga Hydro Ltd uliopo Wilaya ya mufindi mkoani Iringa.

Hayo yamebainishwa leo Julai 31, 2025 wakati wa ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini (REB) ilipotembelea na kukagua mradi wa kuzalisha umeme wa Mwenga Hydro Ltd ambao unatumia nguvu ya maporomoko madogo ya maji (small hydro power potential) ya mto na upepo katika kuzalisha umeme. 

Akizungumza katika ziara hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, Mjumbe wa Bodi, Bw. James Mabula ameeleza kuwa, Rais Samia ametoa zaidi ya shilingi bilioni 15 kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kuwezesha utekelezaji na uzalishaji wa umeme mradi wa Mwenga mkoani humo. 

"Kupitia fedha hizo zinazotolewa na Serikali kupitia REA zinawezesha kuzalisha umeme ambapo megawatt 4 huzalishwa kwa maji, " Amesema Bw. Mabula.

Ameongeza kuwa, hadi sasa jumla ya wateja 8,000 wanapokea huduma ya umeme kutoka mradi wa Mwenga na katika idadi hiyo REA imechangia kuunganishwa kwa wateja wote sawa na asilimia 100.

Kwa upande wake, Meneja wa Teknolojia za Nishati, Mha. Michael Kessy amesisitiza kuwa REA itaendelea kuwezesha mradi wa Mwenga kwa kutoa fedha ili kuuwezesha kuzalisha umeme  wa kutosha na kuwasaidia wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi hususan katika maeneo hayo ya pembezoni. 

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mwenga Hydro Ltd, Deogratius Massawe amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo upo kwenye hatua ya kuongeza wateja wengine wapatao 2,900 kupitia mkataba wa ruzuku ya nyongeza ya fedha zinazotolewa na REA. 

Halikadhalika Bw. Massawe ameishukuru REA kwa kwa kuendelea kutoa ruzuku ambayo imesaidia kuunganisha wateja wanaopatikana katika vijiji vilivyopo katika mkoa wa Iringa.

Ziara hiyo ya Wajumbe wa REB mkoani Iringa imelenga kupitia  utekelezaji wa miradi ya REA inayotekelezwa katika huo sambamba na kupitia changamoto za waendelezaji wadogo wa miradi ya kuzalisha umeme hapa nchini na kupatiwa ufumbuzi.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages