Breaking

Monday, 14 March 2022

AHUKUMIWA MIAKA 30 JELA KWA KUMBAKA MHITIMU WA DARASA LA 7



Na Mwandishi Wetu 

Furaha Samweli Ligate (26) Mkazi wa Kijiji cha Unyangala Wilayani Makete mkoani Njombe amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mara mbili binti mwenye umri wa miaka 15 ( jina linahifadhiwa) aliyekuwa amehitimu darasa la 7 mwaka 2021 akisubiri kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wa 2022.


Hukumu hiyo imetolewa na mahakama ya wilaya ya Makete leo Machi 14, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Ivan Msacky na mwendesha mashitaka Inspekta Msaidizi wa Polisi (Asistant Inspector) Benstad Samson Mwoshe


Imeelezwa kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo la ubakaji Desemba 24, 2021 majira ya saa 12 jioni na kurudia tena Desemba 25, 2021 kinyume na kifungu cha 130 (1)(2)(e) kikisomeka pamoja na Kifungu cha 131(1) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019


Mshtakiwa huyo anadaiwa kumwita chumbani kwake mtoto huyo ambaye anamwita mshtakiwa mjomba na kumbaka kisha kumtishia kumdhuru endapo angesema kwa mtu yeyote .


Mtoto huyo alishindwa kuvumilia na kutoa taarifa ambapo mshtakiwa alikamatwa.

Binti  huyo alipofikishwa hospitali kwa uchunguzi iliguundulika kuwa ameingiliwa kimwili na ni mjamzito


Mwendesha mashitaka wa serikali Inspekta Msaidizi wa Polisi Benstard Mwoshe ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine kwani kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni cha kikatili na kimemuathiri mtoto pamoja na kukatisha ndoto zake za kimasomo.


Akizungumza mahakamani hapo kabla ya hukumu kutolewa mshtakiwa huyo ameiomba mahakama hiyo imuonee huruma na kumpunguzia adhabu kwa kuwa ana familia inayomtegemea ikiwemo mama yake mzazi ambaye ni mzee pamoja na watoto watatu ambao wanamtegemea na amewaacha bila utegemezi wake



Hakimu Mkazi Msacky amesema mahakama hiyo imezingatia maombi ya mshtakiwa ya kupunguziwa adhabu hivyo mahakama hiyo imemtia hatiani kwa kosa la ubakaji na kumhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages