Breaking

Friday, 12 December 2025

WAKALA WA VIPIMO TANZANIA NA ZAMBIA KUSHIRIKIANA KUSIMAMIA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO

Lusaka, Zambia

Taasisi za Wakala wa Vipimo kutoka nchini Tanzania (WMA) na Zambia (ZMA)zimesaini rasmi Mkataba wa kushirikiana katika usimamizi wa matumizi sahihi ya vipimo. Mkataba huo ni wa muda wa miaka mitatu (3) ambapo utekelezaji wake umeanza mara tu baada ya kusainiwa.

Kusainiwa kwa Mkataba huo ni sehemu ya maono ya Viongozi wakuu wa nchi za Tanzania na Zambia ambapo katika siku 100 za uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu kuapishwa kwake amefanikisha utiaji saini baina ya taasisi ya WMA na ZMA kwa lengo la kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji Biashara hususani kwenye sekta ya Vipimo.

Kusainiwa kwa Mkataba huo pia ni matokeo ya ziara ya kikazi ambayo ilifanywa na Wakala wa Vipimo Zambia (ZMA) kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya mafuta nchini humo ambapo wakati wa ziara hiyo walishuhudia namna Serikali ya Tanzania imeiwezesha Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia taasisi yake ya WMA kununua vifaa vya kisasa na ujenzi wa kituo kikubwa Afrika Mashariki na Kati cha kuhakiki Vipimo katika eneo la Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Hafla ya utiaji saini imefanyika Jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 Disemba, 2025 na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali na wataalamu kutoka nchi zote mbili, kwa upande wa Zambia wakiongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Chipoka Mulenga (Mb) na upande wa Tanzania ukuongozwa na Mhe. Lt Gen Mathew Edward Mkingule, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zambia akimuwakilisha Dkt. Hashil T. Abdallah, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara.

Chini ya Makubaliano hayo, mataifa hayo mawili yatatambua matokeo ya vipimo, vyeti vya uthibitisho, idhini za aina (type approvals), na uthibitishaji wa kisheria kutoka upande mmoja hadi mwingine. Mpango huu unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa vikwazo vya kitaalamu katika biashara, kuboresha ulinganifu wa udhibiti, na kuongeza usahihi wa Vipimo katika biashara kwa lengo la kuwalinda walaji kutoka pande zote.

Akizungumza wakati wa ufunguaji wa hafla hiyo Waziri wa Viwanda na Biashara wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Chipoka Mulenga (Mb), ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia taasisi ya Vipimo Tanzania na Zambia kushirikiana katika usimamizi wa Vipimo kwakuwa kumekuwa na sintofahamu kwa muda mrefu kwenye usimamizi wa vipimo baina ya Tanzania na Zambia, ambapo awali kila taasisi ya vipimo haikuwa ikitambua upimaji unaofanywa na mwingine na hivyo kupelekea ucheleweshwaji wa huduma kwa wafanyabiashara na watoa huduma ya uchukuzi katika Ushoroba wa Uchukuzi wa Dar es Salaam na katika vituo vya kutolea huduma ya pamoja mipakani ikiwemo Kituo cha Tunduma/ Nakonde.

“Makubaliano haya yataondoa vikwazo katika biashara na kuchelewa kwa bidhaa katika mipaka yetu kwani kwa sasa bidhaa zitakazokaguliwa na WMA nchini Tanzania zitakubalika na kutambuliwa kutumika nchini Zambia na kadhalika, bidhaa zitakazo kaguliwa na ZMA nchini Zambia zitakubalika nchini Tanzania bila kikwazo.” alisema Waziri Chipoka Mulenga wakati wa hotuba yake.

Makubaliano hayo pia yanabainisha ushirikiano katika mafunzo ya pamoja, utafiti na maendeleo, kubadilishana utaalamu wa kiufundi, na ushiriki hai katika majukwaa ya kikanda na kimataifa ya vipimo kama OIML, SADCMEL, na AFRIMETS. Ushirikiano huu utawezesha taasisi zote mbili kuendelea kuoanisha mbinu bora na teknolojia za kisasa za vipimo zitakazotumika kwa manufaa ya pande zote mbili na kuigwa kikanda.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Lt Gen Mathew Mkingule amesema ushirikiano baina ya taasisi ya Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) na Zambia (ZMA) utasaidia kuondoa malalamiko hasa kwa upande wa wasafirishaji wa bidhaa za mafuta na wamiliki wa vituo vya mafuta ambao kwa muda mrefu wamekuwa kwenye sintofahamu na sasa biashara hiyo inaenda kuimarika zaidi kwakuwa vipimo vitakavyo tumiwa na nchi hizi mbili vitakubalika na pande zote.

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Eliza Mwakasangula Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Vipimo (WMA) amesema Bodi itahakikisha inasimamia utekelezaji wa makubaliano yaliyosainiwa kwa kuhakikisha Mkataba huu unatekelezwa kwa ufanisi, usimamizi na mwelekeo wa kisera unatolewa ipasavyo, mfumo wa ufuatiliaji na tathmini unafanya kazi, uwezo wa kitaasisi, miundombinu na ujuzi vinaimarishwa, pamoja na kuhakikisha ushirikiano unabaki hai kupitia mapitio ya pamoja ya kila mwaka.

“Bodi ya Ushauri ya Wizara itaendelea kuunga mkono Menejimenti kuhakikisha kwamba ushirikiano huu unatoa matokeo yenye tija kwa mataifa yote mawili kwalengo la kuwalinda walaji.” Alisema Prof. Eliza Mwakasangula.

Katika tukio hilo, sekta binafsi ya Jamhuri ya Zambia iliwakilishwa na Chama cha Wasafirishaji wa Petroli cha Zambia Bw. Benson Tembo ambaye aliipongeza Serikali ya Tanzania na Zambia kwa mafanikio yaliyofikiwa kupitia Taasisi hizo za vipimo. Alibainisha kuwa taratibu zilizorahisishwa zitasaidia kuchagiza ukuaji wabiashara ndogo na za kati na hivyo wadau wengi watavutiwa kufanya biashara rasmi, jambo ambalo litasaidia katika kufikia malengo ya biashara za uwili nakikanda mathalani SADC na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Wakala wa Vipimo (WMA) itaendelea kusimamia usahihi wa vipimo wakati wote kwa lengo la kuwalinda walaji kwa kuzingatia miongozo mbalimbali inayotolewa Kikanda na Kimataifa.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages