Breaking

Tuesday, 23 December 2025

WAFANYABIASHARA WA MAZIWA WATAKIWA KUJISAJILI TDB

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WAFANYABIASHARA wanaojihusisha na uuzaji wa maziwa nchini wametakiwa kujisajili katika Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) ili kupata idhini ya kisheria ya kufanya biashara hiyo, huku akionya kuwa kufanya shughuli hizo bila usajili ni kinyume cha sheria.

Wito huo umetolewa  Desemba 23, 2025 jijini Dar es Salaam na Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, George Msalya, wakati wa kikao cha Maandalizi ya Wiki ya Maziwa 2026 kilichowakutanisha wadau wa tasnia ya maziwa nchini.

Msalya amesema kupitia Sheria ya Maziwa namba 8 ya mwaka 2004, Bodi ya Maziwa imepewa mamlaka ya kisheria kuwaondoa au kuwachukulia hatua watu wanaojihusisha na biashara ya maziwa bila kufuata taratibu zilizowekwa, hatua inayolenga kudhibiti madhara yanayoweza kujitokeza kwa walaji na uchumi wa Taifa.

Ameeleza kuwa wafanyabiashara wanaweza kujisajili kwa urahisi kupitia tovuti ya Bodi ya Maziwa kwa kubofya kiungo kinachowaelekeza kwenye mfumo wa MIMS (Milk Industry Management Information System), hatua itakayowasaidia kuepuka adhabu ikiwemo kufungiwa biashara.

Msalya ametaja baadhi ya vigezo vya usajili kuwa ni pamoja na kumiliki ghala la kuhifadhia maziwa kwa wasindikaji, pamoja na kuwa na shamba la mifugo linalotambulika kisheria kwa wazalishaji wa maziwa.

Vilevile ametoa wito Kwa Wadau wa Sekta ya Maziwa nchini kushiriki kikamilifu Maandalizi ya Wiki ya Maziwa ambayo hufanyika kila mwaka mwishoni mwa mwezi Mei huku akibainisha kwamba Kwa mwaka 2026 Maadhimisho hayo yatakuja kivingine kwakufanyika kila Kanda ili kuwezesha wadau wengi zaidi kushiriki tofauti na miaka iliyopita.

Kwa upande wake, Afisa Masoko wa Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza kupitia kiwanda chake cha uzalishaji maziwa Kingolwira-Morogoro (Prisons corpation sole), Glorious masawe amesema ushirikishwaji wa Maandalizi ya Wiki ya Maziwa ni muhimu kwa wadau kwani huongeza umiliki wa tukio lenyewe na kuwa sehemu ya maandalizi.

“Mwaka huu tulishiriki kwa mara ya kwanza Wiki ya Maziwa iliyofanyika Mkoani Morogoro tukapata tuzo ya mzalishaji bora wa maziwa ya daraja la kwanza. Ushiriki wetu katika kikao hiki unatupa mwanga wa kujua maeneo ya kuimarisha nguvu na yale yanayohitaji maboresho katika mnyororo wetu wa thamani,” amesema Bi. Glorius.

Naye Afisa Viwango kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Zena Issah, amesema TBS imekuwa ikishiriki kikamilifu katika maandalizi ya Wiki ya Maziwa ili kuhakikisha uzalishaji wa maziwa bora na salama unazingatiwa, jambo ambalo ni muhimu kwa afya ya mlaji na maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Kwa mujibu wa takwimu, sekta ya maziwa imechangia asilimia mbili ya pato la Taifa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, ikiwa ni chachu muhimu ya shughuli za kiuchumi nchini.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages