Breaking

Monday, 22 December 2025

KATAMBI ASISITIZA UTAFITI WA KISAYANSI KUIMARISHA VIWANDA

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SAALAM

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Partobass Katambi (Mb), amesema Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) ni nguzo muhimu katika kulinda ushindani wa kiuchumi wa Taifa katika mazingira ya uchumi wa dunia yanayoongozwa na sayansi, teknolojia na maarifa.

Akizungumza leo Desemba 22, 2025 jijini Dar es Salaam alipokutana na Menejimenti ya TIRDO, Mhe. Katambi amesema dunia ya sasa inaelekea kwenye ushindani wa kiuchumi unaotegemea ubunifu, uvumbuzi na tafiti za kisayansi, hali inayozilazimu nchi kuwekeza kikamilifu katika taasisi za utafiti ili kujihakikishia maendeleo endelevu.

Amesema maendeleo ya viwanda hayawezi kutenganishwa na sera imara zinazojengwa juu ya ushahidi wa kisayansi, akisisitiza kuwa tafiti zinazofanywa na taasisi za kitaifa kama TIRDO ndizo msingi wa maamuzi sahihi ya kisera na uwekezaji wa kimkakati.

Naibu Waziri huyo ameipongeza TIRDO kwa kuendelea kuimarisha rasilimali watu wake kupitia uwepo wa watafiti wenye shahada za uzamivu, maprofesa pamoja na programu za kujengea uwezo wa kitaalamu, hatua inayoiwezesha taasisi hiyo kutoa ushauri wa kitaalamu unaokubalika katika viwango vya kikanda na kimataifa.

Aidha, amepongeza mchango wa TIRDO katika tafiti zinazolenga uhifadhi wa chakula, maendeleo ya teknolojia za uzalishaji wa viwandani pamoja na kukuza ubunifu wa ndani unaochochea ajira, kuongeza thamani ya bidhaa na kupanua ushiriki wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Mhe. Katambi amesisitiza umuhimu wa kuelekeza tafiti katika kubaini fursa za kufufua au kubadili matumizi ya viwanda vilivyokwama ili viendelee kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na kufanikisha mapinduzi ya viwanda yenye uhimilivu.

Akihitimisha ziara yake, Naibu Waziri huyo ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji unaoendelea kufanywa katika maboresho na ujenzi wa majengo ya TIRDO yaliyoanzishwa tangu mwaka 1984, akisema hatua hiyo inaongeza mazingira bora ya kazi na kuimarisha uwezo wa taasisi hiyo katika kutekeleza majukumu yake ya kitaifa na kimataifa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages