Breaking

Tuesday, 9 September 2025

SHIDA SIYO MOMBO, SHIDA NI AMANI NA UTULIVU WA TANZANIA

 



Septemba 9, 2025

Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam

Hivi karibuni kumekuwa na mtiririko wa taarifa mbalimbali za uzushi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Suleiman Mombo.

Taarifa hizo ambazo zinasambazwa kwa nia ovu na genge la watu waliopo nje ya nchi na wengine wa ndani ya nchi, zinafanya upotoshaji mkubwa kuhusu maisha binafsi na kazi ya mkuu huyo wa taasisi hii nyeti.

Wapotoshaji hao walianza kwanza kusambaza taarifa za uzushi kuhusu kifo cha mkuu wa usalama wa taifa wa Tanzania.

Walivyoona kuwa wameumbuka kuhusu uzushi huo, wakaibua upotoshaji mwingine kuhusu uadilifu wake.

Kwa asili ya kazi yake na maadili ya cheo chake, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (DGIS) hawezi kuitisha mkutano wa vyombo vya habari kukanusha upotoshaji huo.

Mwiko na maadili ya kazi yake yanamtaka akae kimya licha ya shambulio linalofanywa dhidi ya heshima na utu wake.

Je, lengo la kampeni hii chafu ya upotoshaji dhidi ya DGIS ni nini?

Jibu la swali hilo liko kwenye majira ambayo nchi inapitia sasa hivi na mageuzi makubwa ambayo Mombo ameyafanya ndani ya TISS tangu ateuliwe kuongoza idara hiyo mwezi Julai mwaka jana.

Kama ambavyo sote tunafahamu, Tanzania kwa sasa iko kwenye kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu.

Uchaguzi mkuu ni kipindi ambacho TISS inatakiwa kuwa macho pengine kuliko majira yoyote yale ili kuhakikisha utulivu, amani, na maendeleo endelevu ya taifa letu.

Maadui wa Tanzania waliopo nje na ndani ya nchi wanadhani kuwa wakiiteteresha TISS kwa tuhuma za uzushi dhidi ya kiongozi wake mkuu wanaweza kufanikiwa kuibuia taharuki nchini na kuhatarisha ulinzi na usalama.

Mombo anasifika kuwa na ujuzi mkubwa na ubobezi kwenye masuala ya operesheni za ujasusi, ikiwemo kufuatilia na kuzuia vitisho kama vile ugaidi, uhalifu wa kimataifa, na uvamizi wa nje.

Idara ya usalama wa taifa ni moja ya nguzo za msingi za nchi yoyote. 

Idara hii inawajibika kulinda maslahi ya taifa, kuhakikisha usalama wa raia, na kudhibiti vitisho vya ndani na nje vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi. 

Idara ya usalama wa taifa inalinda mipaka ya nchi na kuhakikisha usalama wa kitaifa na kuruhusu raia kuishi kwa amani bila hofu ya vitisho vya usalama.

Idara hii inasaidia kudumisha utulivu wa ndani kwa kupitia usimamizi wa sheria na utulivu, vyombo vya usalama huzuia machafuko, ghasia, na uhalifu unaoweza kusababisha kuvunjika kwa umoja wa taifa. 

Vilevile, idara hii inashirikiana na mamlaka nyingine za serikali kuimarisha mifumo ya ulinzi, kama vile ulinzi wa miundombinu ya umma na taasisi za serikali.

Pamoja na masuala ya usalama, idara ya usalama wa taifa pia ina jukumu la kuchangia uchumi wa nchi kwa kuhakikisha mazingira salama ya uwekezaji. 

Biashara na uwekezaji hustawi pale ambapo kuna amani na usalama, na hii inasaidia kukuza uchumi wa taifa kupitia ajira na mapato ya serikali.

Kwa maana hiyo, idara ya usalama wa taifa ni kiungo muhimu cha maendeleo ya nchi.

Bila usalama wa kitaifa, maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa hayawezi kufanikiwa. 

Ni wajibu wa kila raia kushirikiana na idara hii kwa kutoa taarifa za msingi na kufuata sheria ili kuhakikisha usalama wa taifa unadumishwa.

Hivyo basi, upotoshaji unaofanywa kwenye mitandao ya kijamii siyo shambulio kwa Mombo au TISS peke yake, bali ni shambulio linalolenga kuhatarisha amani, utulivu, usalama, ustawi na mustakabali mzima wa taifa.

Watanzania tusimame imara kuhakikisha kuwa genge la watu lenye nia ovu halifanikiwi kuiyumbisha nchi kwenye kipindi hiki cha uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.

Mungu Ibariki Tanzania.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages