Breaking

Saturday, 23 August 2025

WAFANYAKAZI TARURA DODOMA WAPIMA AFYA, WAPEWA CHANJO YA HOMA YA INI

 

Wafanyakazi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Dodoma wamejitokeza kwa wingi kupima afya na kupata chanjo ya homa ya ini, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wao wa kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kila robo ya mwaka.

Zoezi hilo limefanyika mwishoni mwa wiki katika ofisi za TARURA mkoa wa Dodoma likihusisha uchunguzi wa afya ya moyo, shinikizo la damu, kisukari na saratani pamoja na chanjo ya homa ya ini.

Mratibu wa zoezi hilo kutoka TARURA Dodoma, Ana Semkiwa, alisema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa taasisi kuhakikisha watumishi wanabaki na afya bora na kuepuka madhara ya kiafya yanayoweza kupunguza tija kazini.

“Tunataka kila mfanyakazi awe na tabia ya kujali afya yake kwa kupima mara kwa mara. Afya njema ni msingi wa utendaji kazi bora na maendeleo ya taasisi,” alisema Semkiwa.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Maabara kutoka Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Gideoni Julius, alisema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakiongezeka kwa kasi nchini na hatua ya TARURA ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine.

“Shinikizo la damu, kisukari na homa ya ini yanachangia vifo vingi nchini. Njia bora ya kuyakabili ni kujua hali ya afya yako mapema na kuchukua hatua, ikiwemo chanjo ya homa ya ini ambayo hutoa kinga ya muda mrefu,” alisema Julius.

Aliongeza kuwa jamii inapaswa kuondoa dhana potofu kuwa kupima afya ni kwa wagonjwa pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja ili kujikinga na madhara makubwa.

Mmoja wa washiriki wa zoezi hilo, Agatha Mayaya, alisema amejifunza umuhimu wa kujitokeza kupima afya na kuchanja, akisisitiza kuwa hatua hiyo imempa hamasa ya kuhamasisha wenzake kazini na majumbani.

“Leo nimepata chanjo ya homa ya ini na nimepima magonjwa yasiyoambukiza, sasa nimepata amani ya moyo kwa kujua hali yangu. Naamini kila mtu akijitokeza atajilinda na kulinda familia yake,” alisema

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages