Breaking

Friday, 1 August 2025

NEMC IPO VIWANJA VYA NANENANE DODOMA- MAONESHO YA WAKULIMA




Na.Mwandishi Wetu.


BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki kikamilifu katika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, likitoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira kupitia kilimo rafiki kwa mazingira.

Kupitia banda lake, NEMC inatoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya mazingira, ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kabla ya kuanzisha miradi ya kilimo, ujenzi na shughuli nyingine za kiuchumi.

Aidha, elimu nyingine inayotolewa ni kuhusu,Katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki,Athari za uchafuzi wa vyanzo vya maji,Umuhimu wa kuzingatia kilimo hifadhi,Ulipaji wa ada za mazingira kwa mujibu wa sheria na Elimu ya urejelezaji wa taka kwa ajili ya kulinda mazingira na kuongeza kipato. Maonesho ya Nanenane mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi."

 NEMC imesisitiza kuwa uchaguzi wa viongozi wenye maono katika sekta hizo ni msingi wa utekelezaji wa sera na sheria za mazingira kwa maendeleo endelevu. Baraza hilo limewahimiza wakulima, wafugaji, wavuvi na wananchi wote wanaotembelea maonesho hayo kutembelea banda la NEMC ili kupata elimu sahihi juu ya mbinu bora za kilimo na uzalishaji zinazozingatia utunzaji wa mazingira.

 “Ustawi wa kilimo na uchumi wetu unategemea sana afya ya mazingira yetu. Tunawahamasisha wananchi kufika kujifunza na kushirikiana nasi katika kulinda mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho,” imesema NEMC. Maonesho ya Nanenane kitaifa yameanza rasmi Agosti 1 na yanatarajiwa kufikia kilele chake Agosti 8, 2025.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages