Breaking

Tuesday, 1 July 2025

TTCL YAWAVUTIA WASHIRIKI SABASABA KWA HUDUMA ZA KISASA NA ZENYE TIJA



Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kung’ara katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, kwa kuonesha teknolojia ya kisasa ya mawasiliano inayojibu mahitaji ya sekta mbalimbali nchini.

Akizungumza katika banda la shirika hilo, Meneja wa Banda, Bi. Janeth Maeda, alisema TTCL inatumia fursa ya maonesho hayo kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma zake, huku likijikita katika kutoa suluhisho la mawasiliano lililo salama, la kuaminika na la gharama nafuu kwa Serikali, mashirika na wananchi wa kawaida.

"Huduma zetu zinalenga kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kuhakikisha usalama wa taarifa kwa taasisi na mashirika ya umma na binafsi. TTCL ni mshirika wa maendeleo ya kidigitali nchini," alieleza Bi. Maeda.

Bi. Maeda alisema TTCL imepewa dhamana kubwa na Serikali kusimamia miundombinu nyeti ya mawasiliano kama Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano pamoja na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (National Internet Data Center - NIDC), miundombinu ambayo ni mhimili wa usalama wa taarifa za Taifa na uchumi wa kidigitali.

Amezitaja taasisi zinazofaidika na huduma za TTCL kuwa ni pamoja na wizara zote, mashirika ya umma, sekta za afya, elimu, madini, fedha, usafirishaji, utalii na mashirika yasiyo ya kiserikali.

“Kwa kutumia teknolojia ya fiber optic, tumesaidia taasisi hizi kupunguza gharama, kuongeza kasi ya huduma kwa wananchi na kuimarisha ulinzi wa taarifa zao,” alisema.

Katika msimu huu wa sabasaba, TTCL imetoa punguzo maalum kwa bidhaa za mawasiliano kama routers, USB modems na MIFI, ili kuwapa wateja wake nafasi ya kufurahia huduma bora kwa bei nafuu.

Aidha, TTCL inawaalika wananchi, wawekezaji na taasisi mbalimbali kutembelea banda namba 26 ili kujifunza kwa vitendo kuhusu huduma zake kama uhifadhi wa taarifa kimtandao (data center), mifumo ya TEHAMA, na namna ya kuimarisha mawasiliano ya kiofisi na kibiashara.

“TTCL ni zaidi ya mtandao, ni mshirika wa maendeleo kwa Taifa zima,” alihitimisha Bi. Maeda.





Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages