-Dkt. Kijaji: Watanzania tumieni fursa kupeleka bidhaa Uingereza.
Serikali imewashauri watanzania kutumia fursa ya mpango wa biashara wa Nchi zinazoendelea kwa kuhakikisha wanapeleka bidhaa katika nchi ya Uingereza ili kukuza Uchumi pamoja na pato la Taifa.
Mpango huo mpya umeanza kutumika mwaka jana 2023 ambapo Serikali  ya Uingereza iko tayari kupokea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini  zikiwemo zenye kulipiwa ushuru na zisizolipiwa.
Waziri wa Viwanda na Biashara,Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema hayo leo Dar es Salaam katika semina ya wafanyabiashara  kuhusu fursa ya kuuza bidhaa katika soko la  Uingereza  na Nchi zinazoendelea (UK- DCTS).
Akizungumza Mhe.Dkt. Kijaji amesema  mpango huo  wa bishara na Nchi zinazoendelea  kwa Tanzania umekuja muda muafaka kwa kuwa Nchi   imerekebisha na kuboresha mazingira ya biashara ili kufanya  kukuza kipato na biashara nchini.
Amesema kwa mwaka 2022 mauzo ya Tanzania kwenda Uingereza   yalifikia sh. bil 44 ikilinganishwa na manunuzi ya sh. trilioni 3.08 ya bidhaa kutoka Uingereza.
Amesema kupitia takwimu hizo ongezeko la mauzo kwenda  Uingereza  ni ndogo sana ikilinganishwa na ununuzi wa  bidhaa kutoka Uingereza  Kwenda Tanzania kwani kwa miaka miwili imeongezeka  sh. bilioni mbili  wakati  bidhaa  zilizonunuliwa  ni zenye thamani ya  sh. triloni 1.06.
“Inahitaji nguvu ili kuweza kuvuka na kufikia malengo halisi ya kuanzishwa kwa mpango huo,” amesema Waziri Kijaji.
Aidha, ametolea mfano  taarifa ya Kituo cha Uwekezaji  nchini ( TIC) kuanzia mwaka 1997-2024 jumla ya miradi 980 ya kampuni ya Uingereza  yenye thamani ya Dola za Marekani  milioni 5655.38 zilizotoa ajira za wastani wa  watu 126,322 katika sekta mbalimbali ziliwekezwa  nchini.
“ Tuweze kutumia mpango huo na kuchochea mapato pamoja na fedha za kigeni, lakini pia  kupitia mpango huo Taifa litakuwa na manufaa mbalimbali ambayo ni kupungua kwa masharti ya kupeleka bidhaa na kwa wenye viwanda  ni muhimu kuwa na malighafi  zitakazochochea  ushindani wa bidhaa za Tanzania,” amesema.
Ameongeza pia manufaa ya mpango huo ni  kupungua kwa gharama za kufanya biashara  kurahisisha upatikanaji wa taarifa za masoko kwa Tanzania na hata  kushirikiana na kampuni za Uingereza  kuwekeza na kuzalisha bidhaa bora  Tanzania.
Amehamasisha wafanyabiashara kuona umuhimu wa uadilifu katika kuziona  fursa na kwamba wapeleke bidhaa zinazokidhi soko hilo.
“Serikali yetu ya awamu ya sita imechukua hatua nyingi za kujenga mahusiano ya kidipolomasia na Uingereza  ambapo  Nchi hiyo pia ilianza  kutoa fedha kupitia huduma mbalimbali ambazo zimeelekezwa katika Miradi mbalimbali,” amesema.
Mhe. Dkt.Kijaji ameongeza kuwa  mpango huo umezingatia pia sekta  ya biashara  kwa  kuongeza mchango wa sekta ya biashara katika ukuaji wa viwanda.
Akitoa ujumbe kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania David Cancar amesema  chini ya mpango huo Tanzania ndio yenye bidhaa zinazotakiwa na Uingereza.









 
 
 
 
 
 
 
 
