Taasisi ya Wakala wa Vipimo (WMA) imeandaa na kutoa semina kwa kamati ya kudumu ya Bunge Bukoba Mkoa wa Kagera kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu kazi na majukumu ya wakala hiyo. Katika Semina hiyo wajumbe wa kamati walifahamishwa kazi mbalimbali zinazotekelezwa na WMA ikiwa ni pamoja na Uhakiki wa Dira za Maji, Uhakiki wa Mita za Umeme, usimamizi wa vipimo katika sekta za Mafuta, Gesi, Usafiri na Usafirishaji, Kilimo, Bidhaa zilizofungashwa pamoja na sekta ya Biashara kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Deodatus Mwanyika amesema kuwa taasisi ya Wakala wa Vipimo ni muhimu sana kwenye uchumi kwakuwa inahakikisha wananchi wanapata bidhaa zenye vipimo sahihi na kamati imeelekeza Wizara kuwa na mkakati endelevu wa usimamizi wa vipimo vinavyotumika katika maeneo mbalimbali nchini hususani kuanza mara moja usimamizi wa vipimo katika maeneo ya muda wa maongezi na taxi za mitandao, kwa kuwa maeneo hayo yanalalamikiwa sana na wananchi.
"Sisi kama kamati ya Bunge tunaosimamia na kuishauri Serikali tunnailekeza Wizara  kuwa na zoezi endelevu la ukaguzi wa vipimo sahihi sambamba  utoaji  elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo hasa  kwa wananchi wa chini ambao ndio walaji wa mwisho ili kuhakikisha kiasi cha fedha wanacholipa kiendane na kiasi cha bidhaa wanazonunua " Amesema Mwanyika.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) akichangia katika Semina hiyo ameelekeza Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuzingatia mapendekezo yote   yaliyotolewa na kamati ya Bunge katika Semina hiyo na kutaka utekelezaji wake uanze mara moja ili kuendelea kuwalinda walaji na kuhakikisha wanapata huduma na bidhaa zenye vipimo sahihi wakati wote na kudhibiti matumizi ya vipimo batili.
"Kama Wizara  Kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara tumepokea maelekezo ya  Kamati na michango yote iliyotolewa kwenye Semina hii, naelekeza wataalamu wetu kupitia WMA kuendelea kusimamia matumizi sahihi ya Vipimo na kutoa elimu na mafunzo   mbalimbali kuhusu utumiaji wa Vipimo sahihi  ili Wananchi  wasipunjwe  kupitia  vipimo” ameeleza  Mhe. Exaud Kigahe.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA) Bi. Stella Kahwa ameishukuru kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kwa michango na maelekezo yao waliyotoa kuhusu usimamizi wa vipimo kwenye sekta mbalimbali ili kuhakikisha Wananchi wanapata bidhaa zilizo sahihi wakati wote na vipimo vinavyotumika vinakuwa sahihi wakati wote na pia ameeleza kuwa semina hiyo ni ya siku mbili na Kamati ya kudumu ya Bunge itapata nafasi ya Kutembelea Ofisi ya Wakala wa Vipimo iliyopo kwenye mpaka wa Tanzania na Uganda Mutukula.
Bi. Stella ameeleza kuwa Wakala wa Vipimo ina ofisi katika mipaka mbalimbali Mutukula ukiwa ni mmoja wa mipaka hiyo ikiwa na lengo la kuhakiki usahihi wa bidhaa zote zinazoingia nchini kupitia mipakani ili kuhakikisha bidhaa zinazoingia zinakuwa sahihi wakati wote kwa lengo la kuwalinda walaji na amesisitiza kuwa Wakala itaendelea kufungua ofisi kwenye mipaka mipya itakayoendelewa kufunguliwa kwa ajili ya kuwalinda walaji kwa kukagua mizigo itakayopita kwenye mipaka hiyo ili iwe kwenye vipimo sahihi.















 
 
 
 
 
 
 
 
