Breaking

Monday, 30 May 2022

CHELSEA FC YAUZWA RASMI

Na Said Muhibu, Lango La Habari 
Muungano unaoongozwa na Todd Boehly umefanikiwa kuinunua klabu ya Chelsea kwa kiasi cha dola bilioni 5.2 na kuzika utawala uliopita wa Abrahamovic ambaye aliwekewa vikwazo kuimiliki klabu hiyo na serikali ya Uingereza kufuatia tuhuma za kuhusishwa kuwa na urafiki wa karibu na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu ya Chelsea, muungano unaoongozwa na Todd Boehly, Mwenyekiti na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Eldridge unajumuisha pia kampuni ya uwekezaji ya Clearlake Capital Group inayoongozwa Behdad Eghbali na José E. Feliciano, Hansjörg Wyss, mwanzilishi wa Wyss Foundation, na Mark Walter, mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa Guggenheim Capital. 
Aidha, chini ya makubaliano ya mkataba wa manunuzi Boehly na Clearlake watashiriki umiliki sawa wa klabu wakati Boehly atadumu kama Mwenyekiti au mkuu wa muungano huo.
Boehly na Clearlake wamejitolea kuwekeza katika maeneo muhimu ambayo yatapanua na kuimarisha ushindani wa Chelsea, ikiwa ni pamoja na kuboresha uwanja wa Stamford Bridge, uwekezaji zaidi katika timu ya vijana timu ya wanawake, na uwanja wa Kingsmeadow. 
"Tuna heshima ya kuwa walezi wapya wa Klabu ya Soka ya Chelsea," alisema Boehly.  
"Sote tuko ndani - 100%  kila dakika ya kila mechi.  Maono yetu kama wamiliki yako wazi, tunataka kuwafanya mashabiki wajivunie.  Pamoja na kujitolea kwetu kuendeleza kikosi cha vijana na kupata vpaji bora zaidi, mpango wetu wa utekelezaji ni kuwekeza katika Klabu kwa muda mrefu na kuendeleza historia ya mafanikio ya Chelsea.  Binafsi nataka kuwashukuru mawaziri na maafisa katika serikali ya Uingereza, na Ligi Kuu, kwa kazi yao yote katika kufanikisha hili," aliongezea.
Roman Abramovich amekamilisha uuzaji wa Klabu ya Soka ya Chelsea na kampuni zinazohusiana na kikundi cha uwekezaji kinachoongozwa na Todd Boehly na Clearlake Capital.
Mchakato wa kuiuza Chelsea ulianza mnamo Machi 2, 2022 wakati Abrahamovic alipotangaza nia ya kuiuza klabu hiyo baada ya mafanikio aliyoyapata kwa miaka 19 ndani ya klabu hiyo. Abramovich aliweka bayana kwamba mmiliki mpya lazima awe msimamizi mzuri wa klabu na mapato yote ya mauzo lazima yasaidie waathirika wa vita nchini Ukraine.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages