
Vibanda vya wafanyabiashara wadogo 'Machinga' na mama lishe zaidi ya 30 vimeteketea kwa moto katika Soko la Karume Jijini Dar es Salaam.
Muto huo umeanza leo Ijumaa Aprili 8, 2022 alfajiri na kuunguza maduka ya wafanyabiashara ndogondogo wanaouza mabegi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP. Muliro Jumanne Muliro amekiri kutokea kwa moto huo na kusema chanzo cha moto hakijajulikana lakini uchunguzi unaendelea, japo taarifa za awali zilionyesha kuwa moto ulianza kwenye kibanda kimoja na kisha kusambaa.
"Kwa mazingira yalivyo pale, vibanda vingi vimebanana na vipo kila baada ya hatua mbili, hivyo moto unapotokea ni rahisi kusambaa, bahati nzuri ni kuwa umeshadhibitiwa, na watu wa usalama wapo eneo la tukio," amesema Muliro.
Naye, Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Elisa Mugisha amesema timu yake imeudhibiti moto huo ambao pia umeunguza mabanda ya wafanyabiashara wa mabegi.
Mnamo Januari 16, 2022 Soko la Karume liliteketea kwa moto na kuharibu mali mbalimbali ikiwamo miundombinu ya umeme.
Mnamo Januari 16, 2022 Soko la Karume liliteketea kwa moto na kuharibu mali mbalimbali ikiwamo miundombinu ya umeme.