Breaking

Wednesday, 9 March 2022

WAZIRI UMMY ATOA TAHADHARI YA UGONJWA WA HOMA YA MANJANO


Na Samir Salum - Lango la habari

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa tahadhari ya kuzuka kwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya manjano (yellow fever).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Machi 09, 2022 Waziri Ummy amesema mnamo Machi 03, 2022 Wizara ya Afya ilipokea taarifa kutoka Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyopo hapa nchini, ikielezea kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Manjano nchini Kenya katika County ya Isiolo umbali wa takribani Kilomita 285 Kaskazini mwa Mji Mkuu, Nairobi . 

Amesema taarifa hiyo ilieleza kuwa, mgonjwa wa kwanza mwenye dalili za ugonjwa huu alipatikana mJnuari 12, 2022 na hadi kufikia Machi 03, 2022 kulikuwa na jumla ya wagonjwa 15 na vifo vitatu  vilivyotokana na ugonjwa huu. 

"kati ya sampuli sita  zilizopimwa katika maabara ya Kenya (KEMRI), sampuli tatu  zilithibitika kuwa va virusi vya homa ya Manjano kwa kutumia vipimo vya serology na PCR. Vilevile, kumekuwa na tetesi za kuwa na wagonjwa wenye dalili za homa ya Manjano katika nchi za Uganda, Sudan ya Kusini na Chad" amesema

Akieleza kuhusu uwepo wa ugonjwa huo hapa Nchini Waziri Ummy amesema kuwa taarifa za kipindi cha miezi mitatu iliyopita katika mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa yaliyopewa kipaumbele wa (IDSR) zinaonesha kuwa hapajakuwepo na taarifa zinazoashiria kuwepo kwa ugonjwa wa Homa ya Manjano.

Hata hivyo amewataka wananchi kuchukua tahadhari za ugonjwa huo ambapo amesema kuwa dalili za ugonjwa wa Homa ya Manjano ni pamoja na homa, kuumwa na kichwa, maumivu ya misuli pamoja na mgongo, mwili kutetemeka, kupoteza hamu ya kula, kusikia kichefuchefu na kutapika, mwili kuwa na manjano, kutokwa na damu sehemu za wazi kama mdomoni, puani, machoni na tumboni.

"wakati mwingine damu huonekana kwenye matapishi na kinyesi na ugonjwa unapokuwa mkali figo hushindwa kufanya kazi. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa huu ni kati ya siku 3 hadi 6 baada ya kuambukizwa." amesema

"homa ya Manjano husababishwa na virusi ambavyo huenezwa na mbu aina ya Aedes, kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na vilevile kati ya mtu na mtu huambukizwa kati ya mtu na mtu pindi mtu mwenye virusi hivyo anapoumwa na mbu na hatimaye kueneza kwa mtu mwingine" ameongeza

Waziri Ummy amewaagiza viongozi wa wizara yake kutoa chanjo ya manjano kwa watu wanaosafiri nje ya nchi katika hospitali zote za rufaa za mikoa ili kurahisisha upatikanaji wake. 

Pia ameagiza Hospitali zote za Rufaa nchini kuwa na huduma za kupima na kutoa chanjo ya homa ya manjano kwa wasafiri na wenye uhitaji na pia ameagiza maafisa wa afya mipakani kuhakikisha wasafiri wanaoingia kutoka nchi zenye maambukizi wanakuwa na vyeti vya chanjo. 


Aidha, Wizara imetoa wito wa afya kuendelea kushirikiana katika kutekeleza jitihada mbalimbali za kupambana na magonjwa ya milipuko ikiwepo ugonjwa huu kwa kuzingatia kikamilifu miongozo inayotolewa na imeahidi kuwa itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa magonjwa ya milipuko nchini.

 Mwisho

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages