Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Madini Dkt. Dotto Biteko ameonya watu wanaotegesha katika maeneo ya uwekezaji wa madini kwa lengo la kunufaika na malipo ya fidia.
Waziri Biteko ameyasema hayo Jana Jumatatu Machi 14, 2022 wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi Ibrahim Uwizeye alipofika nchini kwa lengo la kujifunza zaidi kuhusu Sekta ya Madini hususan utekelezaji wa mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya nikeli.
Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wake amesaini Mikataba minne ya wawekezaji katika Sekta ya Madini yenye thamani ya dolla za kimarekani Milioni 738 hivyo wale wanaotegesha kwa ajili ya kulipwa fidia serikali haitawavumilia.
" hawa wanaotegesha hawatalipwa chochote isipokuwa tu kwa wananchi wenye uhalali wa kulipwa" amesema
Akizungumzia lengo la ziara ya Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema imelenga kujifunza kupitia mradi huo ili kuona namna ambavyo nchi hiyo inaweza kujifunza kutoka Tanzania na namna ambavyo nchi hizo zinavyoweza kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya namna hiyo.
“Mradi wa Kabanga Nikeli na Msongati nchini Burundi ni mmoja, jiolojia ya Kabanga na Msongati ni moja na kama mnavyojua jiolojia haina mipaka isipokuwa mipaka ya kiutawala. Pia, wamefika kuona namna nchi hizi zinavyoweza kufanya ili hatimaye ziweze kuwa mfano bora wa ushirikiano kwa mataifa mengine Afrika,” amesema.
Kwa upande wake Waziri Uwizeye amesema ujumbe wake umefika nchini kujifunza ili mradi huo uweze kuzinufaisha nchi zote ikiwemo kuhakikisha nchi hiyo pia inachimba madini hayo na hivyo kuiomba Tanzania kuipa nafasi ya kujifunza kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa jiolojia ya madini hayo pia inapatikana nchini humo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Mathias Kahabi amemhakikishia Waziri Biteko kuwa, Wilaya hiyo haitokuwa kikwazo cha utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa nikeli. Ametumia fursa hiyo kuelezea masuala muhimu matatu ambayo tayari yamefanywa na wilaya hiyo, ikiwemo kufanya zoezi la kutambua maeneo ya kupisha mradi; mazungumzo ya awali kati ya wawekezaji na wananchi katika ngazi zote; na mapitio ya makubaliano ya kuhamisha wananchi.
DC Kanali Kahabi ametumia fursa hiyo pia kumuomba Waziri Biteko kuweka msukumo ili kuwezesha mradi huo kuanza kwa wakati uliopangwa.
Awali, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Tembo Nikeli Benedict Busunzu akiwasilisha taarifa kuhusu mradi huo amesema uhai wa mgodi unatarajiwa kuwa zaidi ya miaka 30 na kuongeza kuwa, tayari Kampuni hiyo imepata mbia mwenza Kampuni ya BHP ambayo ni kampuni kubwa ya madini duniani inayotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kiteknolojia katika utekelezaji wa mradi huo.
Ameitaja teknolojia hiyo kuwa ni ya Hydrometallurgy ikiwa ni ya kwanza kutekelezwa duniani ambayo pia, itakuwa rafiki mkubwa wa mazingira.
Busunzu ameitaja nikeli ya Kabanga kuwa ni ya daraja la juu duniani na kuutaja mradi huo kuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania.