Breaking

Thursday, 10 March 2022

TUME YA MADINI YAENDESHA MAFUNZO KWA WACHIMBAJI WADOGO - MBOGWE



Tume ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira leo  tarehe 10 Machi, 2022 imeanza kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini na  wamiliki wa mitambo ya uchenjuaji wa madini  katika Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe ikiwa ni mkakati wa kuimarisha usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.


 Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira wa Tume ya Madini, Mhandisi Henry Mditi amesema kuwa  maeneo yanayoangaziwa katika mafunzo hayo ni pamoja na usalama migodini, utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya madini usimamizi wa baruti, usimamizi wa mitambo ya uchenjuaji wa madini pamoja na sheria ya madini na kanuni zake.


Ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni pamoja na kuongeza uelewa mpana  wa shughuli za migodi, sheria ya madini hivyo kupunguza matukio  ya ajali kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.


Amesisitiza kuwa mafunzo yameshatolewa katika mikoa ya kimadini ya Mirerani, Chunya, Simiyu, Singida, Dodoma na kusisitiza kuwa mafunzo ni endelevu na yataendelea kutolewa katika mikoa mingine ya kimadini iliyobaki.


Mafunzo hayo yametolewa na wataalam ambao ni viongozi waandamizi wa Tume ya Madini wakiwa ni pamoja na Meneja wa Ukaguzi wa Migodi, Winfrida Mrema, Meneja wa Usimamizi wa Baruti, Mhandisi Aziza Swedi, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Dkt. Anorld Gesase na Afisa Mazingira Mwandamizi, Abel Malulu.


Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe Mhandisi Joseph Kumburu ameongeza kuwa katika kuhakikisha shughuli za uchimbaji wa madini zinaendeshwa kwa kufuata kanuni za usalama na mazingira, ofisi yake imekuwa ikitoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wachimbaji wadogo wa madini.


Amesema kuwa ofisi yake pia imekuwa ikitoa elimu kuhusu sheria ya madini kwenye masuala ya umiliki wa leseni za madini ili kuondoa changamoto ya wananchi kushindwa kutofautisha kati ya umiliki wa leseni ya madini na umiliki wa ardhi ambao umekuwa ukipelekea migogoro ya mara kwa mara.


Aidha, amesema ofisi yake imekuwa ikifanya kaguzi za mara kwa mara kwenye maeneo ya wachimbaji yenye leseni na yasiyo na leseni na kusisitiza kuwa tangu kuanzishwa kwa ofisi yake mapema Julai 2021, jumla ya kaguzi 567 zimefanyika pamoja na kutoa elimu kwa wachimbaji katika maeneo husika.


Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo  hayo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Said Nkumba ameipongeza Tume ya Madini kwa kuandaa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini kwa ajili ya Wilaya za Nyang'wale, Mbogwe na Bukombe na kuwataka wachimbaji wadogo wa madini kufuata miongozo mbalimbali inayotolewa na Tume ya Madini.


Katika hatua nyingine, Nkumba amekemea vikali wachimbaji wa madini wanaoendesha biashara ya madini nje ya mfumo wa masoko ya madini yaliyoanzishwa na Serikali kupitia Wizara ya Madini.


"Katika hili ninatoa onvyo kwa wachimbaji wanaofanya biashara nje ya mfumo wa masoko ya madini yaliyoanzishwa kinyume na sheria, vyombo vya ulinzi na usalama vipo macho, na mtu atakayebainika hatutasita kumkamata na kumchukulia hatua za kisheria," amesisitiza Nkumba


Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyang'wale, Jamhuri William amewataka wachimbaji wadogo wa madini kuzingatia elimu watakayoipata kupitia mafunzo hayo na kusisitiza kuwa wilaya yake ipo tayari kuwasaidia kutatua changamoto watakazokutana nazo


Wakizungumza katika nyakati tofauti, Meneja wa Ukaguzi wa Migodi wa Tume ya Madini, Winfrida Mrema na Meneja wa Usimamizi wa Baruti, Mhandisi Aziza Swedi wamesema kuwa mafunzo husika yana lengo la kutatua changamoto za afya na usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.


"Tupo hapa kwa ajili ya kuhakikisha wachimbaji wanapata elimu ambayo itawasaida kwenye biashara na utunzaji wa baruti bila kuleta madhara kama vile ajali kwenye jamii," amesisitiza Mhandisi Aziza.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wachimbaji wadogo wa madini wamesema kuwa, walikuwa na kiu ya muda mrefu wa kupata elimu hii adimu na kuongeza kuwa sasa wataweza kuendesha shughuli zao kwa kufuata sheria na kanuni za mazingira, kupungua kwa ajali migodini huku Serikali ikiendelea kupata mapato yake.


Katika hatua nyingine wameomba elimu kuendelea kutolewa na kusisitiza kuwa wapo tayari kugharamia mafunzo yote kwa kuwa wamepata elimu ambayo walikuwa wakiisubiri kwa muda mrefu.


"Binafsi mimi nimejifunza namna bora ya usimamizi wa mazingira kwenye shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini pamoja na sheria za madini na ardhi; awali nilikuwa nashindwa kutofautisha kati ya haki ya kumiliki leseni ya madini na hati ya ardhi, binafsi mafunzo haya yamenifungua macho sana," amesema Jumanne Ally ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu katika eneo la Mbogwe.


Katika hatua nyingine wachimbaji wadogo wa madini wamempongeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe, Mhandisi Joseph Kumburu kwa uchapakazi kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini katika eneo hilo na kuongeza kuwa amekuwa akipokea na kutatua changamoto hata usiku inapohitajika.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages