Breaking

Monday, 14 March 2022

RAIS SAMIA KUONGOZA KUMBUKIZI MWAKA MMOJA KIFO CHA MAGUFULI




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kumbukizi ya mwaka mmoja ya kifo cha Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli itakayofanyika katika uwanja wa Magufuli Chato Machi 17, 2022.


Hayo yameelezwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyemule na kuongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na familia ya hayati Magufuli wamekusudia kufanya kumbukumbu ya mwaka mmoja ikiwa ni njia ya kumkumbuka kiongozi huyo.



Ratiba ya kumbukizi itaanza na Misa Takatifu ya kumwombea Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli itakayoanza saa 3.00 asubuhi kwenye uwanja wa Magufuli na kufuatiwa na salamu mbalimbali za viongozi wa Serikali, Chama, Dini na Familia.



Rc Senyemule amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye kumbukizi hiyo ambapo wananchi na wageni wengine wataanza kuingia uwanjani hapo kuanzia saa 12.00 asubuhi.

Baadhi ya viongozi watakaoshiriki hafla hiyo ni makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi pamoja na viongozi mbalimbali wa nchi.


Hayati Magufuli alifariki dunia Machi 17 mwaka 2021 katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es salaam baada ya kuugua maradhi ya moyo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages