Breaking

Thursday, 10 March 2022

MKOA WA KIMADINI MBOGWE WAKUSANYA ZAIDI YA BILIONI 14 ZA MAPATO



Na Samir Salum - Lango la habari 


Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe Mhandisi Joseph Kumburu amesema kuwa ukusanyaji wa mapato umeongezeka  kwa kipindi cha kuanzia mwezi  Julai mwaka jana  hadi   Feburuari mwaka huu nakufikia kiasi cha shilingi Billioni  14.6 .

Mhandisi Kumburu ameyasema hayo leo Alhamisi Machi 10, 2022 kwenye mafunzo ya  wachimbaji wadogo kutoka wilaya tatu za Bukombe,Nyanhwale na Mbogwe  yaliyokuwa yamelenga mada nne ambazo ni elimu ya matumizi ya baruti,usalama na mazingira eneo la uchimbaji,Sheria na usimamizi na malipo ya ukaguzi wa ada za mrabaha.

Amesema kuwa mapato hayo yametokana na mrahaba, ada ya ukaguzi, ada ya leseni na ada ya vibali mbalimbali vinavyohusiana na masuala ya madini.


Aidha Mhandisi Kumburu amesema kuwa Ofisi yake imekuwa ikifanya kaguzi za mara kwa mara kwenye maeneo ya wachimbaji kwa kushirikiana na jeshi la polisi ambapo kuanzia mwezi julai 2021 hadi februari 2022 jumla ya watuhumiwa 75 walikamatwa kutokana na makosa mbalimbali kwenda kinyume na sheria kanuni, taratibu na miongozo ya madini.


Amesema watuhumiwa 22 wamekamatwa katika Wilaya ya Bukombe, 19 wilaya ya Mbogwe na 34 walikamatwa katika Wilaya ya Nyang'wale.


"Jumla ya shilingi Milioni 117 zimekusanywa kutokana na kutozwa faini kwa watuhumiwa hao" Amesema 


Ameongeza kuwa ukaguzi huo umefanyika katika machimbo yenye leseni na yasiyo na leseni na kusisitiza kuwa tangu kuanzishwa kwa ofisi yake mapema Julai 2021, jumla ya kaguzi 567 zimefanyika pamoja na kutoa elimu kwa wachimbaji katika maeneo husika.


Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo  hayo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, amekemea vikali wachimbaji wa madini wanaoendesha biashara ya madini nje ya mfumo wa masoko ya madini yaliyoanzishwa na Serikali kupitia Wizara ya Madini.


"Katika hili ninatoa onyo kwa wachimbaji wanaofanya biashara nje ya mfumo wa masoko ya madini yaliyoanzishwa kinyume na sheria, vyombo vya ulinzi na usalama vipo macho, na mtu atakayebainika hatutasita kumkamata na kumchukulia hatua za kisheria," amesisitiza Nkumba


Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyang'wale, Jamhuri William amewataka wachimbaji wadogo wa madini kuzingatia elimu watakayoipata kupitia mafunzo hayo na kusisitiza kuwa wilaya yake ipo tayari kuwasaidia kutatua changamoto watakazokutana nazo.


Wakizungumza katika nyakati tofauti, Meneja wa Ukaguzi wa Migodi wa Tume ya Madini, Winfrida Mrema na Meneja wa Usimamizi wa Baruti, Mhandisi Aziza Swedi wamesema kuwa mafunzo husika yana lengo la kutatua changamoto za afya na usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.

"Tupo hapa kwa ajili ya kuhakikisha wachimbaji wanapata elimu ambayo itawasaida kwenye biashara na utunzaji wa baruti bila kuleta madhara kama vile ajali kwenye jamii," amesisitiza Mhandisi Aziza.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira wa Tume ya Madini, Mhandisi Henry Mditi amesema kuwa  maeneo yanayoangaziwa katika mafunzo hayo ni pamoja na usalama migodini, utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya madini usimamizi wa baruti, usimamizi wa mitambo ya uchenjuaji wa madini pamoja na sheria ya madini na kanuni zake.


Ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni pamoja na kuongeza uelewa mpana  wa shughuli za migodi na sheria ya madini hivyo kupunguza matukio  ya ajali kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.


Mafunzo hayo yametolewa na wataalam ambao ni viongozi waandamizi wa Tume ya Madini wakiwa ni pamoja na Meneja wa Ukaguzi wa Migodi, Winfrida Mrema, Meneja wa Usimamizi wa Baruti, Mhandisi Aziza Swedi, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Dkt. Anorld Gesase na Afisa Mazingira Mwandamizi, Abel Malulu.






Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages