Na mwandishi wetu - Songwe
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amefanya ziara ya kikazi Mkoani Songwe ambapo ametembelea shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini kwa lengo la kuwatambua wamiliki wa leseni na kutambua changamoto zao.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kiruswa amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Songwe Mhandisi Laurent Mayala ashirikiane na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songwe kukagua na kuzitambua leseni ambazo hazijaendelezwa kwa muda mrefu ili zirudishwe wizarani kwa lengo la kuwapa wachimbaji wadogo wenye uhitaji wa kuchimba.
“Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Afisa Madini naomba mkae muangalie maeneo ambayo yanaviashiria vya madini na yameshikiliwa na leseni za utafiti kwa muda mrefu bila kuendelezwa, mtupe taarifa ili tuyafute na tuwapatie wachimbaji wadogo,” amesema Dkt. Kiruswa.
Dkt. Kiruswa pia amemshauri Mkuu wa Mkoa wa Songwe Omary Mgumba kuwepo na Siku Maalumu ya Maonesho ya Madini katika Mkoa wa Songwe ili kuutangaza Mkoa huo na kuyatangaza madini yanayopatikana mkoani humo.
Dkt. Kiruswa amesema ili kudhibiti utoroshaji wa madini lazima tufungue masoko kwenye maeneo ya kimkakati ili wafanyabiashara wasitoroshe kwenda kutafuta masoko sehemu ambayo yanapatikana.
Aidha, Naibu Waziri ametumia fursa hiyo kuliagiza Shirika la Utafiti la Taifa (STAMICO) kutembelea wilaya ya Songwe kwa lengo la kuwasaidia wachimbaji wadogo ambao wameonekana kuwa na changamoto mbalimbali katika shughuli zao.
Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Songwe Mhandisi Laurent Mayala amesema lengo la Mwaka wa Fedha 2021/22 ni kukusanya Shilingi Bilioni 35 ambapo ndani ya miezi nane ya mwanzo (July 2021 hadi Februari, 2022) ofisi imekusanya bilioni 16.9, sawa na asilimia 72 ya bilioni 23.3 tuliyopaswa kukusanya hadi sasa.
Amesema mauzo katika soko la Madini la Songwe yanaendelea kuongezeka kwani mwezi Disemba, 2021 dhahabu iliyouzwa sokoni hapo ilikuwa kilo113 Matarajio yetu ni kuendelea kusimamia sekta hii ili kulifikia lengo lililowekwa.
Awali, Dkt. Kiruswa alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Omary Mgumba ili kupata taarifa za shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini mkoani humo.