Na Mwandishi Wetu
Imeelezwa kuwa zaidi ya shilingi Bilioni 26 zimetumika kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa mradi wa kisasa wa stendi ya mabasi na malori Nyamhongolo iliyopo katika wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa wilaya ya Ilemela Hasan Elias Masalla wakati akizungumza na washiriki wa mbio za Ilemela maarufu Ilemela Jogging Clubs za Kilomita nane zilizoanzia Buzuruga na kuishia Nyamhongolo stendi ambapo zimejumuisha virabu mbalimbali vya mbio vinavyopatikana mkoani Mwanza.
Dc Masalla amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwaajili ya Utekelezaji wa mradi huo huku akiwaasa wananchi kuutunza.
"Huu ni mradi mkubwa wa stendi ya kisasa Afrika Mashariki inayopatikana wilaya ya Ilemela, Zimetumika zaidi ya Bilioni 26.6 kukamilisha kwake niwaombe tujitokeze kutumia fursa zitakazopatikana" Amesema
Aidha Dc Masala amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Waziri wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwa ushirikiano wake katika kuhakikisha mradi huo unakamilika.
Kwa upande wake mtaalam kutoka Manispaa ya Ilemela Ahmed Sakibu amesema kuwa matangazo kwaajili ya wananchi kujitokeza kuanza kuomba vizimba vya biashara na maduka makubwa ya kisasa yataanza kutolewa kuanzia siku ya Jumatatu kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii.
Sakibu amewaasa wananchi kujitokeza kuomba fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazopatikana pamoja na kuutembelea mradi huo wakati wowote kabla ya kuanza kutumika rasmi.
Fadhili Ramadhan ni Moja ya wananchi waliojitokeza katika kushiriki mbio hizo ambapo amempongeza Mkuu wa wilaya ya Ilemela Kwa ubunifu wake katika kuhamasisha mbio hizo kwani mbali na kusaidia katika kupambana na magonjwa.
" mbio hizi zinasaidia kujikwamua kiuchumi Kwa kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika kutambua fursa za kibiashara na uchumi." Amesema
Wilaya ya Ilemela inaendelea na Utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ya sekta ya afya, Elimu, miundombinu ya Barabara, Maji na huduma nyengine za kijamii.
Mwisho.
TAZAMA MUONEKANO WA STENDI HAPA